Siku moja baada ya kuteuliwa na Rais Dkt. John Magufuli kushika wadhifa huo, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya, Roggers Siang’a, anaye tarajiwa kuapishwa leo kushika wadhifa huo, ameanza kutema cheche, akisema kuna kitu kinakuja kuhusu biashara ya madawa ya kulevya.
Siang’a ameahidi kuwashughulikia kikamilifu baadhi ya wafanyabiashara mkoani Kilimanjaro, wanaodaiwa kuwatumia wanawake wajasiliamali wanaosafirisha mazao kwenda mikoani kubeba mirungi au bangi ndani ya mizigo ya mazao.
Ameyasema hayo katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) baada ya kupewa fursa hiyo na Mkuu wa Mkoa huo, Said Mecky Sadiki, Kamishna huyo amesema kuwa ana mwanga fulani na biashara hiyo na kwamba anayo orodha ya majina ya wafanya biashara wanao wachomekea wanawake hao dawa za kulevya.
”Ninayo orodha ya wafanyabiashara wasio waaminifu na wengine wananchi wa kawaida wanaowatumia wanawake wasio na hatia kusafirisha dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na mirungi na bangi kwenda mikoani, hilo nitahangaika nalo mara ntakaporejea mkoani hapa katika mapambano dhidi ya vitu hivi,” amesema Siang’a.
Siang’a ambaye kabla ya uteuzi ya uteuzi wake alikuwa Ofisa Usalama Taifa, Mkoani Kilimanjaro, ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa kada mbalimbali mkoani humo, watumishi wa umma na wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari wakiwa baada ya kumalizika kwa mazoezi ya viungo kama sehemu ya kuimarisha mwili.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadiki amelitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwaachia baadhi ya wanawake watakaobainika kutokuwa na hatia ama walitumika kusafirisha madawa ya kulevya kwa ridhaa yao.