Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limetangaza kuanzisha kampeni ya kukusanya madeni kwa Wapangaji wa nyumba zake waliopo na waliohama, ili kuhakikisha wanakusanya madeni yanayofikia kiasi cha shilingi 26 bilioni.
Hayo yamesemwa hii leo Oktoba 30,2022 na Meneja wa habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba NHC, Muungano Saguya wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Sirika hilo, yaliyopo eneo la Upanga jijini Dar es Salaam.
Amesema, “Yapo madeni ambayo yanahitaji kufutwa na Bodi ya NHC yanayofikia Shilingi 6 bilioni na pia yapo madeni mapya yaliyojitokeza kutokana na wapangaji waliopo kwenye nyumba ambao wamelimbikiza kodi ya mwezi mmoja hadi sita na yanayoendelea kuongezeka.”
Aidha, Saguya ameongeza kuwa kwa wapangaji waliopo kwenye nyumba na wapangaji waliohama wanaodaiwa malimbikizo ya kodi hadi sasa, wanapewa muda wa siku sitini (60), kuanzia Novemba mosi, 2022 hadi Desemba 30, 2022 kuhakikisha wanalipa malimbikizo yote wanayodaiwa, ili kuepuka kuchukuliwa hatua stahiki.
Hata hivyo, amefafanua kuwa kwa wapangaji waliopo kwenye nyumba ambao hawatalipa deni ndani ya kipindi hicho, Shirika linakusudia kuvunja mikataba yao ya upangaji na kuwaondoa kwenye nyumba kisha kuuza mali zao kwa lengo la kufidia madeni yao.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), hadi kufikia sasa kuna maombi mapya 200 ya uhitaji wa nyumba kila mwezi, ikiwa ni sawa na maombi mapya 2,400 kwa mwaka.