KampuniI ya mawasiliano ya Afrika Kusini ya MTN, imetangaza kufunga maduka yake yote nchini Nigeria kutokana na baadhi ya raia wa Nigeria kulipiza kisasi cha mashambulizi ya kibaguzi yanayofanywa dhidi ya raia wa Nigeria waliopo nchini Afrika Kusini.
Mashambulizi hayo yamemfanya Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Geoffrey Onyeama, kusema kwamba serikali ya Afrika Kusini haijachukua hatua za kutosha kumaliza tatizo hilo.
Aidha, mashambulizi hayo yamewafanya baadhi ya raia wa Nigeria kuchoma moto baadhi ya makampuni ya Afrika Kusini yakiwemo ya MTN, Dstv, na Shoprite.
Kampuni ya MTN imeandika ujumbe kwa wateja wake mtandaoni kuwajulisha kufungwa kwa maduka yake.
Ujumbe huo uliandikwa:
”Yello! Our shops are unavailable today. You can reach us on Twitter- @MTN180, MTNonline.com/Livechat, chat on MyMTN App. For Call Center dial 180.”