Kampuni ya Mafuta ya Total, imekanusha taarifa zilizosambaa mitandaoni kuwa inaondoka nchini kwakuwa imeanza kuuza baadhi ya mali zake.
Mkurugenzi wa Total nchini Tanzania, Marsha Msuya-Kilewo amesema kuwa tetesi hizo zimetokana na hatua ya kampuni hiyo kuuza baadhi ya mali zake, suala ambalo amesema ni utaratibu wa kawaida wa kampuni na halina uhusiano wowote na mpango wa kuondoka nchini.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa uuzwaji wa baadhi ya mali zake una uhusiano wa tukio la Total kununua mali za Kampuni ya Gulf Africa Petroleum Corp (Gapco) mwaka 2017.
Ameiambia The Citizen kuwa baada ya kununua mali zote za Gapco nchini, Total imekuwa na vituo vingi vya kiutendaji ambavyo wakati mwingine vimekuwa vikishindana vyenyewe vinapokuwa vituo vingi katika eneo moja.
“Tulifikia hatua ambayo vituo vyetu vya huduma katika baadhi ya maeneo vilikuwa vinashindana vyenyewe kwa vyenyewe. Uamuzi bora zaidi wa kibiashara katika wakati huo ulikuwa kuuza baadhi ya mali. Lakini kwa ufupi, Total iko Tanzania kwa muda wa kudumu, tupo sana,” amesema.
Madai ya kuwa Total inaondoka nchini yalianza kuenea kwenye mitandao ya kijamii, baada ya kuweka kwenye vyombo vya habari Septemba 1, 2020 kuwa inauza baadhi ya bidhaa zake.