Kufuatia hatua zilizochukuliwa na Serikali ya kusitishwa kwa upatikanaji wa huduma za maudhui ya ndani ya baadhi ya televisheni za nchini kwenye ving’amuzi, wananchi wameomba hatua stahiki kuchukuliwa ili huduma hizo zirejeshwe haraka.
Hata hivyo siku ya Jana ving’amuzi vya Zuku, Azam, MultiChoice na Star Times, vilisitisha kuonesha maudhui kutokea kwenye televisheni za Channel Ten, ITV, Star Tv, EATV, Clouds Tv, asilimia kubwa ya maudhui kwenye televisheni hizo ni ya ndani ya nchi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kulinda sheria na taratibu ambazo mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) imeweka na kutoa wito kwa kila mwenye leseni kuheshimu sheria hiyo na kuzingatia matakwa ya kisheria kwa kutorusha maudhui ambayo hayamo kwenye mkataba.
TCRA hivi karibuni ilitangaza kwenye vyombo vya habari nia yake ya kufungia leseni za kampuni za MultiChoice, Zuku na Azam, endapo zingeendelea kuonesha maudhui ya televisheni za ITV, Channel Ten, EATV, Clouds na Star Tv, kwa kuwa ni kinyume cha sheria na kanuni za leseni zao.
-
LIVE: Katibu Mkuu CCM azungumza na vyombo vya habari, Mbunge mwingine upinzani ajiuzulu
-
Trump aiwekea Zimbabwe ‘kisiki’ kingine kisa uchaguzi
-
Lowassa afunguka madai ya ‘kuwatanguliza watu CCM’
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkazi wa Tabata, Moses Kalue, alisema amekuwa na mazoea ya kuangalia taarifa za habari na habari nyingine kwenye televisheni hizo za ndani ya nchi.
Lakini, tangu jana mchana hakuziona na alipogundua kuwa kuna changamoto za vibali, aliwataka wamiliki wake washughulikie suala hilo mapema.
Mkazi wa Temeke, Ally Hamza alibainisha kuwa, kwa kukosekana kwa televisheni hizo, kutawakosesha huduma ya habari wananchi na kuwataka wamiliki wa televisheni hizo kutafuta suluhu.
Hivi karibuni, vituo vya ITV, StarTv, Clouds Tv, EATV na Channel Ten vilitoa tamko kuiomba serikali iviachie viendelee kutumia ving’amuzi wakati wamiliki wa ving’amuzi wakitafuta suluhu ya sakata hilo, hoja ambayo Waziri Kamwelwe hiyo juzi alisema kuwa haina mashiko.
Amesema, leseni namba moja ya vituo vya televisheni, inavitaka ving’amuzi kutangaza habari, sherehe za kitaifa, matukio ya magonjwa, vipindi vya watoto na sherehe za kitaifa bure bila ya wananchi kulipa, huku nyingine kama mpira wa nje wananchi walipie.
Mwaka 2012 Tanzania ilizima rasmi mitambo ya analojia na kuingia kwenye mfumo wa digitali ambapo ving’amuzi vinne vilishinda zabuni ya kuonyesha chaneli tano za kitaifa bure ambavyo ndivyo vinaruhusiwa kufanya hivyo pekee na kilichotokea sasa ni ving’amuzi visivyokuwa na leseni hiyo kuonyesha pia chaneli hizo.
Aidha Kamwelwe amewahimiza wananchi kutumia ving’amuzi sahihi ili kupata huduma za maudhui ya bila malipo yaani free to air-FTA.