Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewaonya Wanasiasa na baadhi ya watu wanao chukulia tukio la ajali ya Meli ya MV Nyerere kama mtaji wa siasa.
Ameyasema hayo mara baada ya kuwasili katika eneo la tukio kilipozama kivuko cha MV Nyerere huko Ukara, Ukerewe mkoani Mwanza, akitokea mkoani Kigoma ambapo amesitisha ziara yake ya kikazi.
Kangi amesema kuwa serikali inaendelea na zoezi la uokoaji na uopoaji hadi hatua ya kivuko kuondolewa majini, wakiamini bado kuna watu walio hai, huku akiwaonya Wanasiasa na watu wanaochukulia tukio hilo kama mtaji wa kisiasa kuacha kufanya hivyo badala yake watumie nafasi hiyo kuwaunganisha Watanzania.
“Nawaomba wanaochukulia tukio hili kama mtaji wa kisiasa waache mara moja, na waache kuchonganisha serikali na wananchi wake, kwani hatutosita kuwachukulia hatua wale wote wanaochukulia suala hili aidha kwa vitendo au maneno”, amesema Kangi lugola.
Hata hivyo, mpaka sasa watu 209 wamekufa maji katika ajali hiyo huku watu 41 wakiokolewa wakiwa hai, na maiti 172 kati ya 209 tayari zimetambuliwa na ndugu zao.