Kanisa Katoliki nchini Sri Lanka limesitisha ibada zake kwa maelezo ya kujihami na shambulio la kigaidi.
Hatua hiyo imekuja baada ya serikali ya nchi hiyo kuonya kwamba, kuna uwezekano wa taifa hilo kukumbwa tena na shambulio la kigaidi, kama lililotokea siku ya Pasaka tarehe 21 Aprili 2019 katika makanisa matatu na hoteli za kitalii.
Takribani wiki mbili, Kanisa Katoliki limesitisha ibada zake baada ya kutokea kwa tukio hilo lililopoteza maisha ya watu wasio na hatia zaidi ya 250 na kuacha majeruhi kadhaa.
Kanisa hilo lilitoa tangazo la kutofanya ibada Mei 2, 2019 kupitia Msemaji Mkuu wa Dayosisi ya Kanisa Katoliki mji wa Colombo, Kardinali Malcom Ranjith.
Kardinali Ranjith amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba, wamechukua uamuzi huo baada ya kusikia onyo la serikali.
Kabla ya Kanisa Katoliki kusimamisha ibada zake za Jumapili, lilipanga kufanya ibada Jumapili ya jana ya tarehe 5 Mei 2019.