Kiwanda cha karatasi cha China Paper Cooparation Compay Ltd cha mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, kimetoa wito kwa Taasisi za Serikali ikiwemo Baraza la Mitihani la Taifa(NECTA) kutunza karatasi zilizotumika na kuzipelekea kiwandani hapo badala ya kuzichoma moto.
Hatua hiyo inatokana na Kiwanda hicho kutumia karatasi katika uzalishaji bidhaa mbalimbali.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kiwandani hapo Meneja kiwanda hicho, Wilium Mbila amesema mali ghafi kubwa ya kiwanda hicho ni karatasi na kwamba wadau wake wakubwa ni NECTA pamoja na taasisi nyingine za serikali na benki.
“Sisi kama kiwanda tuna nunua karatasi zilizotumika na kuzalishia bidhaa kama karatasi laini (Tishu) ambazo zinatumika katika hoteli mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi, hivyo tunatoa rai kwa taasisi hizo kwamba wasichome karatasi walete kiwandani kwani hatuchukui bure,”amesema Mbila.
Mbila amesema uwekezaji wa kiwanda hicho ni zaidi ya Sh bilion tano na kwamba taka zote zinazozalishwa zinatumika kuzalisha bidhaa.
Aidha, kiwanda hicho kinaiomba serikali kukipatia eneo kubwa la shamba la kupanda miti ya kutengeneza karatasi na bidhaa nyingine zinazotokana na miti.
Amesema hatua hiyo itasaidia kutunza mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo na kwa sasa wananunua miti na magogo kutoka mashamba ya serikali yaliyopo West Kilimanjaro wilayani Siha, Rongai na Rombo.