Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Mhashamu Eusebius Nzigirwa amesema ubunifu wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo umelifanya jimbo hilo kuondokana na utegemezi katika kuwahudumia mapadri na waumini wake ambapo limekusanya zaidi ya bilioni 3.
Askofu Nzigirwa amesema hayo wakati wa ibada ya Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre ya Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Pengo iliyofanyika katika viwanja vya Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Nzigirwa amesema kuwa awali utaratibu wa tegemeza Jimbo ulioanzishwa na Kardinali Pengo, Jimbo hilo lilijikusanyia shilingi milioni 17 tuu kwa mwaka kiasi ambacho hakikutosha kuratibu shughuli mbalimbali za kanisa ikiwemo mahitaji ya mapadre na waseminari wadogo.
“Kardinali Pengo ni zawadi ambayo Mungu ameitoa kwa makusudi yake kwa ajili ya waumini wa Jimbo Kuu la Dar es Saalam, hivyo anapoazimisha miaka 50 ya upadre tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa ajili yake na maisha yake,” amesema Askofu Nzigirwa
Naye Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania, Merek Solczynski amempongeza Kardinali Pengo kwa juhudi zake nyingi katika utumishi wake wa kulihudumia kanisa na jamii kwa ujumla.