Maafisa wa vitengo katika idara mbambali nchini Kenya, watafikishwa Mahakamani wakikabiliw na kashfa ya kuruhusu kwa makusudi uuzaji wa sukari ambayo ilikuwa imetengenezwa kwa matumizi mengine ambayo si salama kwa afya ya binadamu.
Mbali na maafisa hao, pia mfanyabiashara mashuhuri aliyehusika na uagizaji wa sukari hiyo ambaye alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, akitokea Dubai naye atajumuishwa katika mashitaka hayo yanayowakabili watu 20.
Kwa mujibu wa Maafisa wa serikali, wanasema Makontena 40 za sukari yenye sumu, yaliuzwa kwa wakenya licha ya kwamba shirika la ubora wa bidhaa lilikuwa limeagiza kwamba sukari hiyo itumike viwandani pekee.
Mifuko 20,000 ya sukari, kila mfuko ukiwa na uzito wa kilo 50, iliingizwa Kenya mwaka 2018 kutoka Harare, Zimbabwe, lakini ikatangazwa kuwa sukari hiyo ina sumu na hivyo si salama kwa matumizi ya binadamu ambapo hata hivyo inaripotiwa kwamba ilifunguliwa na kuuzwa kwa wakenya.