Serikali Nchini, imesema katazo la matumizi ya kuni na mkaa litazihusu taasisi zote za Umma na Binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku pekee, na si kwa Mwananchi mmoja mmoja kama inavyotafsiriwa.
Akitoa ufafanuzi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji miti kwa kiwango kikubwa na kulinda afya za Wananchi.
Amesema Taasisi zote za Umma na Binafsi zinatakiwa kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2024 wakati zile zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 300 kwa siku zinapaswa kusitisha matumizi ya nishati hiyo ifikapo Januari 31, 2025.
“Bahati mbaya sana baadhi ya watu walitafsiri lile tangazo tulilotoa mwezi wa nne wakawa na wasiwasi kuwa sasa itakuwaje hata mama ntilie au majumbani watashindwa kupika, hapana si hivyo lengo letu ni kuanza kwa taasisi zenye watu wengi,” amesema Jafo.
Jafo ameongeza kuwa, matumizi ya kuni na mkaa yanaathiri afya ya mtumiaji kwa kusababisha magonjwa yatokanayo na kuvuta hewa chafu, ambayo huathiri mapafu, moyo na matumizi ya muda mrefu wa nishati hiyo pia husababisha magonjwa ya Macho.