Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, ametegua kitendawili kuhusu ajira elfu sita za watumishi wa kada ya walimu kama ilivyoamriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwamba waajiriwe walimu ili kukabiliana na uhaba wa watumishi wa kada hiyo hasa kwakuzingatia waliostaafu na walioacha kazi kwa sababu mbalimbali.
Akizungumza jijini Dodoma, wakati wa ziara yake ya kwanza katika Ofisi za Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), ambayo ni moja ya taasisi inayosimamiwa na Ofisi yake, Prof. Shemdoe amesema, utaratibu wa kuajiri utafuata Sheria, Taratibu na Kanuni, huku akionya wale wote walioanza kutumia matapeli kusaka ajira waache mchezo huo mara moja.
Prof. Shemdoe amesema tokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipo ielekeza Ofisi hiyo kufanya mchakato wa kuajiri walimu 6,000 ili kufidia baadhi ya watumishi hao kwa sababu mbali mbali, kumezuka wimbi la matapeli na wengine kuwadanganya watu wanaoomba ajira kwamba watawasaidia kupata ajira hizo.
“Nimepata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa, wapo baadhi ya watu kwa nia ovu wamekuwa wakiwatapeli kwa kuwaomba fedha baadhi ya walimu wanaotaka kuomba ajira na kuwataka watoe pesa ili zifikishwe Wizarani kwa ajili ya kuwapatia ajira, nipende kusema wazi kwamba jambo hili halipo,” amesema Prof. Shemdoe.
Ameongeza kwamba, vishoka wote watakaobainika kutekeleza utapeli huo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo vya dola, huku akiwataka wale wote watakaokumbana na adha hiyo kutosita kutoa taarifa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika chombo hicho kinachoangalia nidhamu ya watumishi walimu, Katibu Mkuu, Shemdoe amewataka watumishi wa ofisi hiyo kutoa ushirikiano kwa Katibu Mtendaji aliyeteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni kushika wadhifa wa Ofisi hiyo.