Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amekuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi kuhusu tukio la walinda amani wa Umoja huo kwenye ujumbe wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO kuua raia na kujeruhi wengine mpakani mwa nchi hiyo na Uganda.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric ameeleza hayo jijini New York, Marekani wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Dujarric amesema “Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu ametoa salamu za rambirambi na pia ameomba radhi kwa tukio la jana ambalo lilihusisha walinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Kasindi mpakani mwa DRC na Uganda.”
Amesema Katibu Mkuu amemjulisha Rais Tshisekedi kuwa Umoja wa Mataifa umejizatiti kwenye suala la amani na kuratibiana na kushirikiana na jeshi la DRC, FARDC kutatua hali ya sasa na kuleta utulivu mashariki mwa taifa hilo la maziwa makuu.
“Mazungumzo ya dhati na ya kweli yanahitajika,” amesema Katibu Mkuu akiongeza “na kwa hilo kufanyika tunataka kuondoka DRC kwa kikundi cha M23 bila masharti yoyote na vikundi vyote vilivyojihami vikomeshe aina zote za ghasia.”