Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kukomeshwa kile alichokiita “ukatili” wa polisi nchini Nigeria, ambayo imekumbwa na maandamano kwa wiki mbili sasa.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, Guterres amevihimiza vikosi vya usalama kujizuia kwa wakati wote na kutoa wito kwa waandamanaji kuandamana kwa amani na kujiepusha na machafuko.
Guterres amesema watu waliokuwa na silaha ambao waliwafyatulia risasi za moto waandamanaji wa amani jana usiku mjini Lagos, walisababisha vifo kadhaa na majeruhi wengi.
Wakati huo huo, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel amelaani mauaji ya waandamanaji akitoa wito wa kupatikana haki.
Katika hatua nyingine Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limedai watu wasiopungua 12 wameuawa wakati vikosi vya serikali vilipowafyatulia risasi waandamanaji katika eneo la Lekki Mjini Lagos.
Shirika hilo limesema uchunguzi umebaini ushahidi wa vifo 12 huku mamia wakijeruhiwa.
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zimeitaka mamlaka nchini Nigeria kuchunguza na kuwawajibisha waliohusika na matukio hayo.