Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amejivunia kuwa na kikosi imara kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kusuasua msimu uliopita na kufikia hatua ya kuchunguliza shimo la kushuka daraja.
Katwila kwa kushirikana na benchi la ufundi amefanya usajili wa wachezaji kadhaa, ambao anaamini watakiwezesha kikosi chake kuwa kwenye ubora wa kupambana wakati wote, pindi msimu wa 2020/21 utakapoanza mwishoni mwa juma hili.
Katwila amesema wamefanya usajili kwa kuzingatia uwezo wa wachezaji na mapungufu waliyokuwa nayo kwenye kikosi chao.
Kocha huyo mzawa amesema, licha ya kuamini kuwa amefanya usajili mzuri, bado amekua akiwahimiza wachezaji hao kuhakikisha wanatoa mchango mzuri kwa ajili ya kutimiza malengo.
Amesema kwa kushirikiana na benchi lake la ufundi walifanya tathimi ya kina na kujiridhisha wachezaji waliowahitaji wana viwanago vya kuitumikia Mtibwa Sugar msimu ujao, hivyo hawana budi kuushukuru uongozi wa klabu kwa kuwatimizia mahitaji ya kuwapata.
“Sisi hatukusajili tu. Tumesajili wakati ligi inaendelea, kwa hiyo tulikuwa tukiviona vipaji na uwezo wa wachezaji wakati mechi zinaendelea, tukajua tukimchukua fulani na fulani wanaweza kufaa na kuingia haraka kwenye mfumo wetu, hivyo tuna imani yao na tunajivunia pia,” alisema Katwila, mchezaji wa zamani wa timu hiyo.
“Labda mtu mwenyewe tu ashindwe kuzoea mazingira ambayo yamebadilika kutoka kwake, lakini kila kitu kiko sawa na tuko tayari kwa ligi,” Amesema Katwila.
Wachezaji waliosajiliwa Mtibwa Sugar katika kipindi hiki ni Geofrey Luseke, Hamad Hilika, Aboubakar Ame, Kassim Khamisi, Hassan Kessy na Abdul Haule ambaye amepandishwa kutoka kikosi cha vijana.