Kaya 1600 katika vijiji kumi mkoani Njombe zinatarajiwa kupata umeme wa uhakika mara baada ya kukamilika kwa mradi wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia maporomoko ya maji wa Luponde Hydro Ltd unaotekelelezwa na kampuni ya Rift Valley Energy.
Hayo yamesemwa na Meneja Mradi wa Luponde Hydro, Mugombe Maxwell katika ziara ya wataalamu wa Nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika Mkoa wa Njombe ili kujionea maendeleo ya miradi midogo ya umeme wa maporomoko ya maji na nishati jadidifu inayotekelezwa katika mkoa huo.
Maxwell amesema kuwa kampuni ya Rift Valley Energy ina miradi miwili ambayo ni Mwenga Hydro Grid wenye uwezo wa Megawati 4.1na Luponde Hydro Ltd utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 3 mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wake hivyo kuwezesha vijiji kumi katika mkoa huo kupata umeme wa uhakika ifikapo mwakani.
Akizungumzia mradi huo wa Luponde Hydro Ltd, Maxwell amesema kuwa mradi ulianza mwaka 2016 na kuongeza kuwa mradi huo upo katika maeneo mawili ambayo ni Luhololo na Igola yote yakiwa mkoani Njombe.
Maxwell amesema kuwa mradi huo umegawanyika katika awamu mbili na kuendelea kusema kuwa awamu ya kwanza inahusisha usambazaji wa umeme wa uhakika katika vijiji saba vyenye kaya 1120, shule tisa na vituo vya afya vitano
Aidha,ameongeza kuwa, awamu ya pili inahusisha usambazaji wa umeme wa uhakika katika vijiji vitatu vyenye kaya 180.
Vile vile amesema hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi huo katika eneo la Luhololo imekamilika kwa asilimia 60 kwa kazi za kawaida na asilimia 40 katika ujenzi wa mitambo.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa lengo la mradi ni kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na umeme wa uhakika na kuchangia ukuaji wa uwekezaji kwenye viwanda hususan katika maeneo ya vijijini, hivyo kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi