Kaya 1600  katika vijiji kumi mkoani Njombe  zinatarajiwa kupata umeme wa uhakika mara baada ya kukamilika kwa mradi wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia maporomoko ya maji wa Luponde Hydro Ltd unaotekelelezwa na kampuni ya  Rift Valley Energy.

Hayo yamesemwa na Meneja Mradi  wa Luponde Hydro, Mugombe Maxwell katika ziara ya wataalamu wa Nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika Mkoa wa Njombe ili kujionea maendeleo ya miradi midogo ya  umeme wa maporomoko ya maji na nishati  jadidifu inayotekelezwa katika mkoa huo.

Maxwell amesema kuwa kampuni ya Rift Valley Energy ina miradi miwili ambayo ni Mwenga Hydro Grid wenye uwezo wa Megawati 4.1na Luponde Hydro Ltd utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 3 mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wake hivyo kuwezesha vijiji kumi katika mkoa huo kupata umeme wa uhakika ifikapo mwakani.

Akizungumzia mradi huo wa Luponde Hydro Ltd, Maxwell amesema kuwa mradi ulianza mwaka 2016 na kuongeza kuwa mradi huo upo katika maeneo mawili ambayo ni Luhololo na Igola yote yakiwa mkoani Njombe.

Maxwell amesema kuwa mradi huo umegawanyika katika awamu mbili na kuendelea kusema kuwa awamu ya kwanza inahusisha usambazaji  wa umeme wa uhakika katika  vijiji saba vyenye kaya 1120, shule tisa na vituo vya afya vitano

Aidha,ameongeza kuwa, awamu ya pili inahusisha usambazaji wa umeme wa uhakika katika  vijiji vitatu vyenye kaya 180.

Vile vile amesema hatua iliyofikiwa ya  utekelezaji wa mradi huo katika eneo la  Luhololo imekamilika kwa asilimia 60 kwa kazi za kawaida na asilimia 40 katika ujenzi wa mitambo.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa lengo la mradi ni kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na umeme wa uhakika na kuchangia  ukuaji wa  uwekezaji kwenye  viwanda  hususan katika maeneo ya vijijini, hivyo kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi

Magazeti ya Tanzania leo Machi 8, 2017
Makala: Siku ya wanawake duniani na changamoto zake