Kocha mkuu wa Young Africans Cedric Kaze amesema wachezaji wake wapo tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa 18 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons, utakaochezwa Alhamisi, Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, keshokutwa Alhamis (Desemba 31).
Kikosi cha Young Africans tayari kimeshawasili mjini Sumbawanga kwa ajili ya mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini Tanzania, hasa baada ya mabingwa hao wa kihistoria kuweka rekodi ya kutopoteza mchezo wowote tangu walipoanza harakati za kusaka ubingwa msimu huu 2020/21.
Kocha Kaze amesema anatambua mchezo dhidi ya Tanzania Prisons utakua mgumu na wenye upinzani mkubwa, lakini amewaandaa wacheaji wake kupambana na hali hiyo, ili kutimiza lengo la kuondoka na alama tatu muhimu.
Amesema kila mchezo wa Ligi Kuu ni mgumu, hasa wanapokua ugenini kutokana na timu nyingi kucheza kwa kukamia, pindi wanapokutana na kikosi chake.
“Wachezaji wapo vizuri na mazoezi ambayo wameyafanya ni mazuri yananipa picha kwamba tunakwenda kupata matokeo ugenini,”
“Ninatambua mchezo utakua mgumu na upinzani mkali sana, lakini nimewahimiza wachezaji wangu kupambana kama walivyofanya kwenye michezo iliyopita, tutakua ugenini na itatulazimu kucheza kwa malengo makubwa ya kuondoka na alama tatu.”
“Unajua timu nyingi zimekua na tabia ya kucheza na Young Africans kwa kukamia, hilo nimeshaliona na nimelichukua kama changamoto katika kuwandaa wachezaji wangu.” Amesema kocha Kaze.
Young Africans itaanza mbilinge mbilinge za mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu kwa kukusanya alama 43 zinazowaweka kileleni, na keshokutwa itanza mzunguuko wa pili ikiwa na lengo la kuendeleza ushindi.
Mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Dar es salaam Uwanja wa Mkapa, Tanzania Prisons walilazimisha sare ya kufungana bao moja kwa moja.