Kocha Mkuu wa Young Africans, Cedric Kaze amekasirishwa na hatua ya baadhi ya wachezaji wake kuitwa kwenye timu zao za taifa, ili hali wakiwa bado hawajapona kikamilifu majeraha yaliyokua yakiwakabili.
Wachezaji Saido Ntibazonkiza Dickson Job waliokuwa majeruhi kwa muda mrefu, ni sehemu ya wachezaji waliotajwakwenye vikosi vya timu zao za taifa ambazo mwezi huu zitakua na jukumu la kucheza michezo ya kuwania kufuzu fainali za Afrika.
Saido na Job walisajiliwa kwenye dirisha dogo, japo mshambuliaji huyo kutoka Burundi alishaanza kuitumikia timu hiyo tofauti na mwenzake, wote walikuwa majeruhi na kushindwa kuitumikia timu yao, lakini juma lililopita waliitwa kwenye timu za taifa za Burundi na Tanzania.
Kitendo hicho kimemchefua Kocha Kaze, akidai kujumuishwa kwa wachezaji hao katika timu hizo za taifa wakiwa bado hawajawa fiti, kimemchanganya.
Job ameitwa kikosi cha Tanzania, Taifa Stars na Kocha Kim Poulsen kwa ajili ya michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Kenya na nyingine mbili za kuwania kufuzu fainali za Afrika (AFCON 2022), huku akiwa hajaichezea klabu yake mchezo wowote tangu asajiliwe kwa sababu ya majeraha.
Job aliumia akiwa kwenye kambi ya Stars, ikijiandaa na michuano ya Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ 2021, iliyomalizika hivi karibuni nchini Cameroon, wakati Saido ameitwa kwenye timu ya taifa lake la Burundi.
Kaze amesema baada ya Job kuumia alitibiwa na Young Africans, hivyo kocha Poulsen alipaswa kuwasiliana naye ili kupata taarifa ya mchezaji huyo.
“Job ndio kwanza ameanza mazoezi ili kujiweka fiti tayari ameitwa tena, wakati hajacheza mchezo hata mmoja, simpingi kocha Poulsen pengine anataka kumuangalia kwa karibu, lakini hilo halizuii kupata taarifa kutoka kwangu ili kumpa programu zake ili akirejea ndani ya timu asianze upya,”
“Saido ni majeruhi hajacheza muda mrefu najiuliza mbona kaitwa kwenye timu yake ya taifa, laiti kama makocha wangeniuliza ningewapa taarifa za wachezaji hao,” amesema Kaze akihofia kuwapoteza kwa muda mrefu wachezaji hao endapo wataumia wakiwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa.
Kikosi cha Young Africans kimeshaanza safari ya kuelekea mjini Tanga, tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union, utakaochezwa keshokutwa Alhamis.
Young Africans imekuwa ikipata wakati mgumu ikicheza Uwanja wa Mkwakwani Tanga. Hata mchezo wao wa mwisho msimu uliopita uliisha kwa suluhu, licha ya kupata ushindi inapocheza jijini Dar es Salaam dhidi ya Wagosi wa Kaya.
Mara baada ya mchezo wa Alhamisi, Young Africans itasafiri hadi mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kucheza na Polisi Tanzania moja ya timu inayowasumbua kila wanapokutana, huku vijana wa Kaze wakitakiwa kukomaa ili kulinda rekodi yao ya kutopoteza katika Ligi kwani tangu walipolazwa 1-0 na KMC Machi 12, 2020 wamecheza jumla ya michezo 33 bila kupoteza.