Tume ya kupambana na ufisadi nchini Kenya (EACC), imewasilisha katika bunge la Senate ushahidi unaoonesha namna shirika la usambazaji dawa nchini humo (KEMSA), lilivyohusika kwenye sakata la ufujaji wa mabilioni ya fedha za kununua vifaa vya kupambana na janga la Corona.
Tume hiyo iliyokabidhi ripoti yake kwa mkurugenzi wa mashataka nchini humo Noordin Haji mwishoni mwa wiki iliyopita, ilianza uchunguzi wake baada ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuamuru matumizi ya pesa za kupambana na janga la Corona kuchunguzwa kufuatia malalamiko kutoka kwa umma.
Katika ripoti yake ambayo ilikabidhiwa bunge la Senate, EACC imesema KEMSA imeshindwa kueleza kwa ushahidi tosha, namna shilingi bilioni saba nukta nane zilizovyotumika.
Maafisa wa ngazi za juu katika shirika hilo wamebainika kuhusika kwenye ununuzi wa vifaa vya kimatibabu kwa gharama ya juu na ukiukaji mkubwa wa sheria za ununuzi wa serikali.
Katika ripoti nyingine ya mamlaka ya kutathmini manunuzi ya serikali, KEMSA inadaiwa kununua kwa mfano dawa za Paracetemol na vitakasa mkono kwa bei iliyo juu mara mbili,wakati huu wa janga la Corona.
Kenya ikiwa imeshuhudia migomo ya kila mara ya wafanyakazi katika sekta ya afya wakilalamikia kukosa vifaa maalum vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya Corona wanapokuwa kazini.
Kamati ya pamoja kutoka bunge la kitaifa na lile la Senate bado wanaendelea kufanya uchunguzi wao kuhusu sakata hilo.