Imefahamnika kuwa Beki wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Kennedy Juma, ameshonwa nyuzi sita, kufuatia jeraha alilolipata kwenye mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/22 dhidi ya Dodoma Jiji FC.

Kennedy alilazimika kukimbizwa hospitali, baada ya kupigwa kiwiko na Mshambuliaji wa Dodoma Jiji FC Anuar Jabir, katika dakika ya 43 ya mchezo huo uliounguruma Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Ijumaa (Oktoba Mosi).

Hata hivyo Mshambuliaji huyo aliadhibiwa kwa kuoneshwa kadi nyekundu, kwa kosa la kupiga kiwiko.

Mtu wa karibu na daktari wa Simba, Yassin Gembe, amethibitisha taarifa za kushonwa nyuzi sita kwa beki huyo ambaye alichukua nafasi ya Joash Onyango, aliyeumia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Young Africans Septemba 25.

“Jicho la Kennedy lilivimba kabisa, ile ilikuwa ni rafu mbaya sana ambayo alichezewa na yule mchezaji wa Dodoma, ililazimika ashonwe nyuzi sita ili kuweza kukaa sawa,” amesema mtu huyo.

Mtu huyo aliongeza kuwa Kennedy alilia na kusikitika sana baada ya kupata majeraha hayo kwa sababu alijua nafasi yake ya kwenda kambi ya timu ya Taifa imeingia mchanga.

“Kennedy alilia na kuumia sana moyoni kwa sababu hiki ndiyo kipindi ambacho alikuwa anaaminiwa timu ya Taifa Stars, sasa maumivu yake.”

Katika mchezo huo Simba SC ilichomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wao Dodoma Jiji FC, ukiwa ni ushindi wa kwanza kwa Mabingwa hao wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22.

Azam FC yasaka mbinu za kuibanjua Pyramis FC
Dawa ya covid-19 yapatikana! Wataalam Marekani wasema ‘sio muujiza’