Benchi la Ufundi la Simba SC limeongeza matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Simba SC itaanzia ugenini kati ya Oktoba 15 na 16, kisha watamalizia nyumbani jijini Dar es salaam, Uwanja wa Benjamin Mkapa kati ya Oktoba 22 na 24.

Matumaini ya kufanya vizuri kwenye michezo hiyo ya nyumbani na ugenini yameongezeka kufuatia kurejea kwa kiungo Mshambuliaji kutoka Ghana Bernard Morrison, ambaye alikosekana kwenye michezo ya awali ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ngao ya Jamii.

Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomes amesema kurejea kwa Morrison kutaongeza morari kwenye kikosi chake, na atamtumia ipasavyo kuanzia kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy na Ligi Kuu ambapo mchezo ujao watapapatuana dhidi ya Polisi Tanzania.

“Michezo mitatu iliyopita imekuwa ya faida kubwa kwetu kutuandaa na mashindano mbalimbali tutakayoshiriki mwaka huu, kwa namna ninavyokiona kikosi changu nashawishika kusema tupo tayari.”

“Tuna mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika michuano ambayo ni muhimu kwetu, lazima tujiandae kufanya vizuri katika hatua hii na ni jambo zuri kuona tuna nafasi ya kumtumia tena Bernard Morrison katika mashindano hayo.” amesema Gomes

Morrison alifungiwa kucheza michezo mitatu na Shirikisho la soka nchini TFF, kufuatia utovu wa nidhamu aliouonyesha baada ya mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho dhidi ya Young Africans uliopigwa mjini Kigoma, Uwanja wa Lake Tanganyika.

Mali ya siri ya familia ya Uhuru Kenyatta yafichuliwa
Magori aongoza mapambano ya ubingwa Simba SC