Mshambuliaji wa Young Africans, Kennedy Musonda amefunga mabao mawili katika Ligi Kuu Tanzania Bara tangu asajiliwe dirisha dogo, lakini hiyo haijamzuia kuandika Rekodi ya kibabe.
Mzambia huyo, alifunga bao kwenye mechi iliyoipa Young Africans ubingwa wa ligi kwa msimu huu dhidi ya Dodoma Jiji, iliposhinda kwa mabao 4-2, na kumfanya nyota huyo kutwaa taji la pili la ligi akiwa na timu mbili tofauti msimu mmoja.
Musonda amekuwa mchezaji wa kwanza kutoka Zambia kushinda mataji mawili ndani ya msimu mmoja akianza Ligi Kuu ya Zambia akiwa na Power Dynamos, kisha sasa na Young Africans kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Young Africans dirisha dogo akitoa Power Dynamos FC ameliambia gazeti hili kuwa amekuwa mchezaji mwenye furaha kubwa kutua timu yenye malengo na kutwaa taji huku akiwa na ndoto ya kuandika rekodi ya kubeba taji la Afrika.
“Tumetwaa taji tukiwa na michezo miwili mkononi na tunakwenda kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Marumo tukiwa kwenye hali nzuri ya ushindani na malengo yetu ni kutinga fainali.
“Haitakuwa rahisi, tunatarajia ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani wetu kama walivyotushangaza nyumbani, hatukutarajia kukutana na ushindani kama waliotupa, hivyo tumejiandaa vyema kwa kutambua tunakutana na timu ya aina gani.” amesema.
Musonda amesema malengo ya wachezaji na benchi la ufundi ni kuona wanapata matokeo mazuri na kutinga fainali kwa heshima huku akisisitiza kuwa kwa walipofikia kila mchezo wanaocheza wanauchukulia kama fainali.
“Young Africans ni timu ambayo kutokana na matokeo mazuri tunayoyapata tunakutana na changamoto ya kukamiwa na wapinzani mchezo uliotupa ubingwa. Mechi ya kesho Jumatano, kama tutapata bao mapema tutamaliza mchezo,” amesema