Zaidi ya familia 600 zimeachwa bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji ya mafuriko katika vijiji vya kata za Witu, Mkunumbi na Hongwe, Kaunti ya Lamu.
Katika kata ya Witu, nyumba 87 za kijiji cha Moa zimesombwa, nyumba 70 kwenye kijiji cha Cha Laluma na 56 katika kijiji cha Dide Waride zilikuwa zimezingirwa na maji yanayosababishwa na kuvunjika kwa kingo za Mto Tana na ule mdogo wa Nyongoro kutokana na mvua kubwa ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika maeneo hayo.
Kulingana na ripoti ya Shirika la Msalaba Mwekundu, tawi la Lamu, jumla ya familia 445 zimeathiriwa na mafuriko katika vijiji hivyo.
Mwenyekiti wa Nyumba Kumi kijijini Chalaluma, Bonea Abadima, ameeleza wasiwasi wake kwamba huenda wakaambukizwa maradhi yanayosababishwa na maji machafu yaliyozingira nyumba zao.
“Vyoo vimebomolewa na mafuriko. Wakazi wa hapa wanatumia maji hayo hayo kwa matumizi ya nyumbani, Kuna hatari ya mripuko wa kipindupindu wakati wowote hapa,” amesema Abadima.
Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia amesema ofisi yake pamoja na wadau wengine tayari wameanza harakati za kusambaza chakula cha msaada kwa waathiriwa wa mafuriko hayo.