Maofisa wawili wa mamlaka ya mapato nchini (TRA) wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, (TAKUKURU) Mkoani Manyara, kwa kudaiwa kupokea rushwa ya shilingi milioni 10.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu amesema maofisa hao wanadaiwa kufanya kosa hilo kinyume cha kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007. 

Makungu amewataja majina yao kuwa ni Subilaga Mwangama na Ojungu Mollel, amesema wanatarajiwa kufikishwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi wa wilaya ya Babati na kusomewa mashtaka na waendesha mashtaka wa TAKUKURU, Isdory Kyando akisaidiana na wakili Martin Makani. 

Ameeleza kuwa wanadaiwa kupokea rushwa hiyo baada ya kumuomba mfanyabiashara wa mjini Mbulu, (jina linahifadhiwa) ambaye ni mlipa kodi mzuri kwenye ofisi za TRA Mbulu. 

“Mfanyabiashara huyo alilipa kodi ya shilingi milioni tisa mwaka, 2018 hata hivyo Machi mwaka huu akapigiwa simu na watuhumiwa akitakiwa kufika ofisi za TRA mjini Babati,” ameeleza Makungu. 

Alipofika mjini Babati watuhumiwa hao wawili walimwambia wamefanya uchunguzi na kugundua kuwa alikadiriwa vibaya hivyo alipe ongezeko la shilingi milioni tano. 

Amesema hata hivyo mfanyabiashara huyo alikubali na kuanza kulipa ongezeko hilo kwa awamu baada ya kuruhusiwa na meneja wa TRA wilayani Mbulu. 

“Mfanyabiashara huyo baada ya kulipa awamu ya kwanza ya fedha hizo alipigiwa simu tena na watuhumiwa hao na kutakiwa kuonana nao Babati juu ya ulipaji wa kodi wa mwaka 2018 waliomaliza kujadili,” ameeleza Makungu. 

Amesema alipofika mjini Babati maofisa hao wa TRA walimwambia kuna ongezeko la kodi ya shilingi milioni 45 kwenye biashara yake. 

Ongezeko hilo lilimweka mfanyabiashara huyo kwenye wakati mgumu ndipo wakampoza kuwa watampunguzia hadi shilingi milioni tisa endapo angekubali kuwapa rushwa. 

“Walijadiliana kiasi cha kutoa rushwa ili apunguziwe ndipo akaelezwa atoe shilingi milioni 10 akaelekezwa kuzipeleka kwa mawakala waliopo mjini Babati ndipo TAKUKURU wakaweka mtego na kuwakamata watuhumiwa,” ameeleza Makungu. 

Aidha ametoa wito kwa TRA kuangalia upya mfumo wa ulipaji kodi ili kuondoa mianya ya maofisa wake kuwabambikia wafanyabiashara kodi kisha kuwatishia kwa rushwa kama watuhumiwa hao walivyofanya. 

Bigirimana kutua Afrika Kusini
Van Persie: Van Gaal alinichapa kofi 2014