Kenya inapanga kuwarudisha nyumbani wanafunzi 85 ambao wamekwama katika mji wa Wuhan nchini China ambapo ndio kitovu cha mlipuko wa virusi vya Corona na kuwatenga punde tu watakapowasili ili kufuatilia afya zao.
Waziri wa Afya nchini humo ameiambia kamati ya afya ya bunge kwamba wanafunzi hao watarejeshwa nchini Kenya pindi China itakapoondoa zuio la usafiri katika mji huo.
“Waziri wa mambo ya nje anawasiliana mara kwa mara na wanafunzi 85 wa Kenya” Dkt. Mercy Mwangangi amesema hayo bungeni.
“Tumetenga vyumba viwili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na kutenga chumba cha kufuatilia wagonjwa katika hospitali ya Kenyatta. Pia vituo zaidi maalum vimetengwa katika kaunti ya Nairobi,” ameongeza.
Bado haijafahamika iwapo zuio la usafiri katika mji wa Wuhan litaondolewa lini lakini nchi kadhaa zimekuwa zikihamisha raia wake walioko kwenye mji huo. Misri ilikuwa nchi ya kwanza kuchukua hatua hiyo.
Shirika la Afya Dunia (WHO) limesema kwamba lina wasiwasi kuhusu jinsi nchi za Afrika zilivyojitayarisha kukabiliana na virusi hivyo.
Jumanne, Dr Michel Yao – maneja wa kukabiliana na hali za dharura barani Afrika kutoka (WHO), alisema nchi nyingi za Afrika zina mfumo dhaifu wa Afya.
Dkt. Yao amesema kwamba kuna maabara sita pekee barani Afrika zenye uwezo wa kuchunguza virusi vya Corona ambazo ni Nigeria, Ghana, Madagascar, Sierra Leone na Afrika Kusini.
“Afrika Kusini imefanya vipimo 71 vya ugonjwa huo kutoka nchi mbalimbali ambavyo vilikuwa vinashukiwa kuwa ugonjwa wa Corona. Hata hivyo vipimo vyote vimeonyesha kwamba visa hivyo siyo vya Corona,” Dr Yao amesema.
Shirika la Afya Duniani limesema kwamba litatoa usaidizi kwa nchi 24 ili ziweze kufanya utafiti wa visa vya ugonjwa huo ambavyo hadi kufikia sasa vimesababisha vifo vya watu 426 nje ya China.
Hadi kufia sasa Afrika haijathibitisha kisa chochote cha ugonjwa huo.