Serikali ya Kenya inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta imeandaa muswada wa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio nchini humo.
Rais Kenyatta amesema kuwa mabadiliko hayo yataondoa pengo lililopelekea mpinzani wake, Raila Odinga kuyakosoa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya IEBC, kuhusu baadhi ya matokeo kutoka vituoni kutowasilishwa kwenye tume hiyo kwa njia ya kielektroniki.
Amesema kuwa mabadiliko hayo yataeleza kuwa matokeo yawasilishwe kwa njia ya kielektroniki na njia ya kawaida ya kutumia masanduku ya kura (manually), Alifafanua kuwa inapotokea matokeo yamewasilishwa kwa njia mojawapo kati ya hizo, njia ya kawaida itakuwa na nguvu zaidi ya ile ya kielektroniki.
Moja kati ya hoja zilizompa ushindi Raila Mahakamani katika kesi ya kupinga ushindi wa Rais Kenyatta ni Tume kumtangaza mshindi wakati matokeo ya vituo 11,000 hayakuwa yamewasilishwa kwa njia ya kielektroniki.
Hata hivyo, kambi ya upinzani ya NASA inayoongozwa na Raila imepinga hatua hiyo ya kutaka kubadili kipengele kwenye sheria ya uchaguzi.
Asasi za Kiraia na wananchi kwa ujumla wamepewa siku 10 za kutoa maoni yao kwenye kamati maalum ya Bunge kuhusu mabadiliko hayo kabla ya kuwasilishwa rasmi bungeni.
Kenya inajiandaa kufanya uchaguzi wa marudio mwezi ujao baada ya Mahakama ya Juu nchini humo kubatilisha matokeo ya uchaguzi uliofanyika Agosti 8 mwaka huu, yaliyompa Rais Kenyatta ushindi wa asilimia 54.