Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemjibu aliyekuwa mshindani wake mkuu kwenye uchaguzi wa urais wa nchi hiyo uliomalizika wiki iliyopita, Raila Odinga kufuatia tamko lake la kuwataka wakenya kususia kwenda kazini akiwataka kuomboleza ‘uchakachuaji’ wa matokeo ya uchaguzi huo.
Akizungumza leo mchana, Rais Kenyatta ambaye alitangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo kuwa mshindi kwa asilimia zaidi ya 54 amemwambia Raila na wafuasi wake kuwa anawapa mkono wa urafiki kati kati yao ili waendelee kuijenga nchi hiyo kwani muda wa uchaguzi umekwisha.
Rais Kenyatta pia amesema kuwa Wakenya wameamua kuwa uchaguzi umekwisha na kwamba wengi wao wamejitokeza kwenda makazini na kuachana na wito wa kususia kazi uliotolewa na kiongozi wa upinzani.
“Kwa wale rafiki zetu ambao bado hawajakubali matokeo, tunaendelea kuwasihi. Tunawapa mkono wa urafiki… kama kuna ambao wanaendelea kutoridhishwa na uchaguzi kuna njia za kikatiba ambazo wanaweza kuzifuata,” alisema Rais Kenyatta.
Rais Kenyatta pia aliwataka polisi wa nchi hiyo kufanya kazi kwa kuweka mipaka, lakini alisisitiza kuwa Serikali haitaruhusu maisha ya watu kupotea pamoja na uharibifu wa mali.
Kwa mujibu wa BBC, mitaa ya Nairobi leo imeonekana kuanza kurejea katika hali ya kawaida tangu Agosti 8 ambapo Wakenya walifanya uchaguzi Mkuu. Biashara zimerejea katika hali yake ya kawaida katika maeneo mengi.