Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amekanusha taarifa zilizotolewa na mmoja kati ya wawakilishi wa BBC kuwa wakenya wanaweza kutumika katika majaribio ya dawa ya virusi vipya vya corona (covid-19).
Mwakilishi wa BBC, Fergus Walsh alieleza katika mahojiano na kituo hicho kuwa timu ya wataalam wa afya kutoka Chuo Kikuu cha Oxford wanatengeneza dawa ambayo inaweza kujaribiwa nchini Kenya kama haitafanikiwa nchini Uingereza.
Mkuu huyo wa nchi amesema kuwa taarifa hizo ni za uzushi na za kupuuzwa, akieleza kuwa Wakenya hawatatumika kama wanyama katika majaribio hayo, bali timu ya wataalam nchini humo imeungana na jitihada za dunia nzima za kutafuta dawa ya kinga ya virusi hivyo.
“Baadhi ya watu wanasema kwenye mahojiano kuwa kuna utafiti unaendelea na kwamba Wakenya watatumika kama wanyama kujaribu dawa ya kinga. Madai hayo ni uongo mtupu,” alisema Rais Kenyatta alipolihutubia taifa, leo, Aprili 25, 2020.
“Naomba wanaotoa taarifa msisababishe taharuki na woga baina ya Wakenya wenzetu,” aliongeza na kufafanua kuwa Serikali itatoa taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa na wataalam wa nchi hiyo.
Hadi Aprili 25, 2020, kulikuwa na visa 343 vya corona nchini Kenya, wagonjwa 98 wanaendelea vizuri na vifo 14 vilivyosababishwa na virusi hivyo.