Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS), una wasiwasi wa kuongezeka kwa kesi za unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro inayoibuka licha ya kupungua kwa jumla kwa idadi ya raia walioathiriwa na ghasia nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Juba nchini Sudan Kusini na UNMISS, imesema ripoti ya hivi karibuni ya Haki za Kibinadamu waliyoitoa ikiangazia robo ya pili ya mwaka 2022, ilirekodi vifo vya raia 922 ikiwa ni sawa na kupungua kwa asilimia 15 kwa waathiriwa, ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2021.
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Nicholasa Haysom amesema wasiwasi unatokana na ongezeko la asilimia 218 la unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro.
“Ongezeko kubwa la unyanyasaji wa kingono na kijinsia halikubaliki kabisa, na linawaathiri vibaya zaidi wanawake na wasichana. Ghasia hizi zinazogawanya jamii na kutatiza maridhiano zinafaa kukomeshwa,” amesema Haysom.
UNMISS, imesema inaunga mkono mamlaka kuhakikisha kuna uwajibikaji na upatikanaji wa haki kwa walionusurika na waathiriwa kupitia mahakama mbalimbali, kama vile uamuzi wa kesi za ubakaji kupitia mchakato wa Mahakama Kuu ya Kivita huko Yei, Jimbo la Equatoria ya Kati.
Kama ilivyokuwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu 2022, migogoro baina ya jamii iliendelea kuwa chanzo kikuu cha madhara ya raia na kusababisha asilimia 60 ya vifo vya raia, wakati asilimia 38 ya vifo vilisababishwa na vikosi vya serikali na Vuguvugu la Ukombozi wa Watu wa Sudan. /Jeshi, wa upinzani ni SPLM/A-IO ambao wanazidi kutegemea wanamgambo washirika kushiriki katika migogoro.
Hata hivyo, UNMISS imeitaka Serikali ya Sudan Kusini kuchunguza kwa haraka ukiukaji wa haki za binadamu na kuwawajibisha wahusika na kutoa wito wa kuhakikisha kuna utekelezaji kikamilifu wa mkataba wa amani ili kuwezesha sekta ya usalama kutekeleza jukumu la msingi la Serikali la kulinda raia.