Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Vincent Mashinji amesema kuwa wao kama chama ndio wadhamini wakubwa wa ubunge wa Tundu Lissu kwani hawezi kuwa mbunge bila kuwa mwanachama.

Ameyasema hayo jana jijini Dar es salaam mara baada ya kusogezwa mbele kwa kesi ya maombi iliyofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Singida Mashariki kupitia chama hicho, Tundu Lissu.

Amesema kuwa kitendo cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kumvua ubunge aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu umekiathiri pakubwa chama hicho.

”Kama mnavyojua Katiba ya nchi inasema huwezi kugombea cheo chochote cha Kiserikali kama hujadhaminimwa na chama cha siasa, kwa hiyo Lissu anatokana na Chadema, hivyo kuvuliwa ubunge wake ni maamuzi ambayo yamekiathiri chama, hivyo na sisi tutasimama naye bega kwa bega, tukutane Agosti 23 siku itakayosomwa tena kesi yake,”amesema Mashinji

Kwa upande wa mdogo wake Lissu, Vincent Mughwai amesema kuwa wao kama familia wapo pamoja na ndugu yao ambaye hajarudi nchini kutokana na kuendelea na matibabu nchini Ubelgiji.

Amesema kuwa wanawashukuru Watanzania na waandishi wa habari na wanaendelea kuomba ili haki iweze kutendeka katika shauri hilo lililofunguliwa mahakamani hapo.

Kuhusu kurudi nyumbani kwa Tundu Lissu, Mghwai amewataka Watanzania kuwa wavumilivu ambapo muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi kuhusu ujio wake, lakini akasema kitu cha msingi ni ubunge wake.

 

Video: Spika Ndugai aomba muda kujibu hoja za Tundu Lissu, JPM, Ramaphosa watangaza neema
Huyu ndugu yetu ameonyesha uthubutu mkubwa- Mizengo Pinda