Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amesitisha uamuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, uliotolewa jana Agosti 14, 2019 ambapo watumishi wote 137 wa Hospitali ya Mji wa Bariadi walitakiwa kukatwa mishahara yao kwa ajili ya kuchangia fedha ya kununua mashine ya ULTRASOUND, iliyoibiwa katika wodi ya wazazi hospitalini hapo badala yake ameagiza vyombo vya dola vifanye uchunguzi kubaini aliyeiba mashine hiyo na hatua stahiki zichukuliwe.

Sagini ameyasema hayo leo Agosti 15, 2019 wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi katika Ukumbi wa Hospitali hiyo Mjini Bariadi.

Amesema kuwa uongozi wa Mkoa umetafakari na kuona kuwa si watumishi wote wa hospitali hiyo wamehusika katika upotevu wa mashine hiyo kwa kuwa wanafanya kazi katika idara tofauti na baadhi yao siku ya tukio hawakuwepo, hivyo ni vyema vyombo vya dola vikafanya uchunguzi kubaini waliohusika.

”Uongozi wa Mkoa tunarekebisha baadhi ya hatua zilizochukuliwa na DC Kiswaga, hili jambo haliwezi kuwa la watumishi wote 137, kama Serikali tunavyo vyombo vya dola ambavyo kuna watu wanalipwa mishahara kwa kazi hizo za kiuchunguzi, tunataka kifaa hicho kirejeshwe, vyombo hivi vifanye uchunguzi, vichukue hatua kwa watakaobainika ikiwemo kupelekwa mahakamani,”amesema Sagini

Katika hatua nyingine Sagini amewataka watumishi wa Hospitali ya Mji wa Bariadi kuimarisha mfumo wa makabidhiano ya kazi na vifaa vya kazi ili kuwepo na taarifa sahihi za wagonjwa na vifaa tiba kama utaratibu unavyotaka.

Kwa upande wao watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi wamewashukuru viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa kusitisha uamuzi wa awali ambao ungewaathiri kiuchumi na kupunguza ari ya kufanya kazi hususani wale ambao hawajahusika na upotevu wa mashine hiyo.

” Tunamshukuru sana kiongozi wetu kwa msamaha aliotutolea kwasababu tangu jana tumelala kwa presha baada ya kuambiwa kuwa kila mtu alipe, mimi uwezo wangu mdogo na mshahara wangu ni mdogo nilikuwa sioni pesa ya kulipa hicho kifaa, namshukuru Mungu kwa uamuzi wa viongozi wa mkoa yaani naongea kwa uchungu mpaka nasikia kulia kwa furaha niliyonayo” amesema Frola Katoyo Mtumishi katika idara ya dawa.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mkoa wa Simiyu, Catherine Nyingi amesema kuwa Chama hicho kinaushukuru uongozi wa mkoa kwa kutambua sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma na wameiomba Serikali iendelee kuwa macho katika kusimamia sheria, kanuni na taratibu.

Mashine ya kupima magonjwa ya ndani ya mwili wa Binadamu (ULTRASOUND MACHINE) iliripotiwa kuibiwa katika Wodi ya wazazi katika Hospitali ya Mji wa Bariadi Agosti 05, 2019 na jana Agosti 14, 2019 Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga akaagiza watumishi wote 137 wa Hospitali hiyo wakatwe fedha kwenye mishahara yao ili mashine hiyo iliyoibiwa inunuliwe.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 16, 2019
Skimu 100 za umwagiliaji zanufaika na mafunzo nchini