Kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demeokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe imeahirishwa hadi Agosti 6, 2021 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Wakili Peter Kibatala ambaye anamwakilisha Mbowe amesema kesi hiyo imeshindwa kusikilizwa kwa mara nyingine kwa njia ya video conference kutokana na tatizo la mtandao.
Hali kadhalia Wakili Kibatala amewaeleza wanahabari kuwa kesi hiyo itaendelea kesho ambapo wamekubaliana kwa kesho washtakiwa hao watafika Mahakamani.
“Teknolojia imefeli hivyo tumeshindwa kufanikisha mchakato huo kwa sababu kumekuwa na mawasiliano hafifu kati ya ‘video conference facility’ za hapa katika Mahakama ya Kisutu na Gereza la Ukonga na tumekubaliana kwamba kesho washitakiwa waletwe mahakamani,” amesema Kibatala
Awali Mbowe alifikishwa katika Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Julai 26 na kusomewa mashtaka mawili ikiwemo la kula njama za kutenda uhalifu kosa ambalo anadaiwa kulitenda kati Mei na Agosti 2020 katika Hoteli ya Aishi iliyokoko mkoani Kilimanjaro.
Katika shitaka la pili mshitakiwa huyo anadaiwa kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi kosa ambalo anadaiwa kulitenda katika tarehe tofauti mwezi Mei na Agosti 2020 katika eneo lililotajwa hapo awali.