Katika kesi inayomkabili Mkurugezi Mtendaji wa Kampuni ya Jatu Public Limited, Peter Gasaya (32), anayekabiliwa na shitaka la kujipatia fedha tasilimu Sh bilioni 5 kwa njia ya udanganyifu, umedai upelelezi haujakamilika.
Kwa mujibu wa Habari leo Gazeti mtandao Wakili wa serikali Tumaini Maingu, ameeleza hayo leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Francis Mhina.
Maingu amesema kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Wakili wa utetezi Kung’he Wabeya, aliiomba mahakama ahirisho fupi kwa sababu wanataka kuwasilisha hoja kuhusu dhamana ya mteja wao.
Baada ya kusikiliza maombi hayo Hakimu Mhina aliahirisha kesi hiyo na mshitakiwa ataendelea kubaki rumande hadi Januari 13, mwaka huu.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka inadaiwa kuwa katika terehe isiyofahamika kati ya Januari Mosi na Desemba 31, mwaka 2021 ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jatu Public Limited, alijipatia Sh 5,139,865,733.00 kutoka Saccos ya Jatu, akijinasibu kukizalisha kiasi hicho cha fedha kwa kuwekeza fedha katika kilimo cha faida, wakati akijua si kweli.