Watangazaji watatu wa Homeboyz Radio ya Kenya wamesimamishwa kazi na kipindi chao kimefungiwa na Mamlaka nchini humo, baada ya kutoa maoni yaliyodaiwa kumkandamiza muhanga aliyenyanyaswa kingono.
Watangazaji hao, Shaffie Weru, Joseph Munoru (DJ Joe Mfalme) na Neville Musya walikuwa wanazungumzia kesi inayoendelea mahakamani ambapo Eunice Wangari anamtuhumu Moses Gatam Njorogekwa waliyekutana Facebook kwa kumsukuma nje ya dirisha wakiwa kwenye jengo hilo refu, walipokutana kwa mara ya kwanza, baada ya mwanamke huyo kukataa kushiriki ngono.
Watangazaji hao walikosolewa zaidi kwenye mitandao ya kijamii kwa kumlaumu muhanga wa tukio hilo ambaye hivi sasa ni mlemavu.
Mamlaka nchini Kenya zimekifungia kipindi hicho na kueleza kuwa maoni ya watangazaji hao yalilenga katika kutukuza unyanyasaji wa wanawake.
Katika kipindi hicho, mtangazaji Shaffie Weru alihoji baada ya kusimulia kesi hiyo, “mnadhani wanawake wa Kenya wanapatikana kirahisi, wanajirahisisha sana, wanatamaa sana na ndio sababu wanajikuta wanakamatika kwenye hali kama hiyo?”.
Baada ya kipande cha kipindi hicho kusambaa mtandaoni, Wakenya waliwakosoa vikali ikiwa ni pamoja na watu maarufu.
“Mazungumzo haya ni machafu. Hii sio njia sahihi ndugu zangu. Kuwadhalilisha wahanga ni upumbavu kama kilivyo kitendo chenyewe cha unyanyasaji. Boresheni,” aliandika msanii wa kundi la Sauti Sol, Bien-Aimé Baraza
Alhamisi wiki hii, ikiwa ni siku moja tu baada ya kipindi kuruka, makampuni ya matangazo yaliondoa matangazo yake kwenye kituo hicho cha radio.