Mashauri ya kudai talaka miongoni mwa wanandoa yanaongoza katika idadi ya kesi zinazofunguliwa na kusikilizwa katika mahakama maalumu inayotembea na kutoa huduma katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana Jijini Mwanza.
Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo ya Mkuyuni Jijini Mwanza, Jennifer Nkwabi amezungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa tangu mwaka 2019 kesi 502 zimefunguliwa Mahakamani hapo, kati ya hizo kesi 200 ni za kudai talaka.
“Kesi zinazoshika nafasi za juu katika mashauri yaliyofunguliwa mbele ya Mahakama inayotembea ni za mashauri ya ndoa, watu kudaiana fedha na mirathi,” Amesema Hakimu Nkwabi.
Aidha mratibu wa Mahakama hiyo ambayo pia inafanya shughuli zake Jijini Dar es Salaam Moses Ndelwa, amesema kuwa hadi kufikia Mei 2021, jumla ya kesi 1,208 zimefunguliwa katika mkoa yote miwili, huku kesi 520 zimeshasikilizwa na kumalizika, halikadhalika watu 13,668 wamehudumiwa na mahakama inyotembea.
Sambamba na hayo Mahakama inakusudia kukuza huduma hiyo hadi vijijini hasa katika maeneo yasiyi na huduma za kimahakama ikiwemo Wilaya za Butiama, Rorya mkoani Mara, Gairo mkoani Morogoro, na Chemba mkoani Dodoma.
Aidha Mratibu wa Mahakama Ndelwa amesema Mahakama hiyo imepata mafanikio makubwa.