Kiungo kutoka Ghana Kevin-Prince Boateng amefikisha idadi ya klabu 12, tangu alipoanza kucheza soka, baada ya kukamilisha usajili wa kujiunga na Besiktas, inayoshiriki ligi kuu ya Uturuki.
Klabu ya Besiktas inakua klabu ya nne kwa Boateng ndani ya misimu miwili, akitangulia kuzitumikia Fiorentina na Sassuolo zote za Italia, na kabla ya hapo alikua mchezaji halali wa mabingwa wa soka Hispania FC Barcelona msimu wa 2018-19.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32, pia amewahi kucheza katika ligi ya England na Ujerumani, katika kipindi cha miaka 15 iliyoshuhudia akicheza soka katika kiwango cha juu.
Klabu nyingine alizowahi kuzitumikia ni Hertha BSC, Portsmouth, Schalke 04, Las Palmas, Eintracht Frankfurt, AC Milan, Tottenham na Borussia Dortmund na ilidhaniwa wakati alipojiunga na FC Barcelona mwezi Januari mwaka 2019, huenda angedumu kwa muda mrefu klabuni hapo, lakini aliambulia kucheza michezo minne pekee, akiwa na miamba hiyo ya Liga.
Akiwa na klabu ya Fiorentina tangu mwanzoni mwa msimu huu, amecheza michezo 15, na kufunga bao moja.
Licha ya kuzaliwa nchini Ujerumani, Boateng aliamua kuichezea timu ya taifa ya Ghana, huku kaka yake Jerome Boateng, akifanya uchaguzi tofauti, kufanikiwa kuwa sehemu ya wachezaji waliotwaa ubingwa wa dunia mwaka 2014.
Boateng akiwa na kikosi cha Ghana alibahatika kucheza michezo 15.