Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi, amekiri kufurahishwa na hatua ya kurejea mazoezini kwa Kiungo kutoka nchini Uganda Khalid Aucho.
Kwa muda wa siku kadhaa Aucho amekua nje ya kikosi cha Young Africans, ambacho kinaendelea na harakati za kutetea mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Kocha Nabi amesema, kiungo huyo tangu Jumamosi amekua akifanya mazoezi binafsi baada ya kupona majeraha yake, na anaamini kurejea kwake mazoezini kutaongeza changamoto kwa wachezaji wengine wa Young Africans.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema, amefurahia hatua hiyo kwa sababu Aucho ni mchezaji muhimu, ambaye ataongeza kitu kwenye harakati zao wa kupambania ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.
“Nimefurahi kuona kikosi changu kikiwa imara kutokana na uwepo wa baadhi ya wachezaji ambao walikosekana katika michezo iliyopita kwa ajili ya majeraha.”
“Kati ya hao ni Aucho ambaye amepona majeraha yake yaliyomsababisha aikose michezo iliyopita.”
“Kiungo Aucho alianza mazoezi mepesi ya binafsi kwa ajili ya kujiweka FIT zaidi na michezo ijayo. Kurejea kwake kutaimarisha kikosi changu pamoja na kuongeza changamoto kwa wachezaji wengine.” amesema Nabi
Aucho ameanza mazoezi mepesi chini ya uangalizi wa madaktari wa Klabu ya Young Africans, ambao wanachukua tahadhari zote ili kiungo huyo asijitoneshe majeraha yaliyomuweka nje kwa muda wa siku kadhaa.