Beki wa kushoto kutoka nchini Uganda Mustapher Kiiza anatajwa kukaribia kujiunga na Klabu ya Young Africans, ambayo imejizatiti kufanya usajili kabambe kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu na michuano ya Kimataifa.
Kiiza ambaye amewahi kunolewa na Mshambuliaji wa Zamani wa klabu za AS Monaco, Arsenal, FC Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa Thiery Henry alipokua kiinoa klabu ya Montreal ya Canaca, atajiunga na Young Africans kufuatia mkataba wake kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa za awali zinadai kuwa Kiungo kutoka nchini Uganda Khalid Aucho ambaye ni miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha Young Africans msimu huu, amekua chagizo kubwa la kumshawishi Kiiza kujiunga na Vinara hao wa Ligi Kuu.
Kiiza mwenye umri wa miaka 22 aliyeibuliwa na KCCA ya nchini kwao Uganda, atakua mchezaji huru siku kadhaa zijazo, hivyo Young Africans watampata kirahisi, kupitia dirisha la usajili ambalo litafunguliwa rasmi baada ya msimu huu 2021/22 kufikia kikomo.
Kinachosubiriwa kwa sasa upande Uongozi wa Young Africans ni Beki huyo wa kushoto kutua jijini Dar es salaam, akitokea nchini Canada ambako kwa sasa anaendelea kufungasha vilivyo vyake kwa ajili ya kurejea Barani Afrika.
“Kiiza anakuja Tanzania, anakuja Young Africans baada ya mabosi kumtengea bajeti iliyonona, ni beki mwenye uwezo mkubwa na amewahi kufanya kazi na Henry, kabla ya kocha huyo kuteuliwa kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ubelgiji mapema mwaka jana,” kimeeleza chanzo cha taarifa kutoka ndani ya Young Africans.
“Atakuwa mchezaji huru wakati wowote kuanzia sasa, kufuatia mkataba wake kuwa ukingoni, kwa kiwango alichonacho kinachompa nafasi ya kucheza katika timu ya taifa ya Uganda, kinampa na nafasi ya kuja kuingia moja kwa moja katika mipango ya kocha, kwani msimu ujao tutashiriki michuano mikubwa na tunahitaji kuwa na kikosi chenye wachezaji bora.”
Beki huyo anayesifika kwa kukaba kwa nguvu na akili sambamba na kutengeneza mashambulizi na mkali wa kupiga krosi zenye macho, alianza kucheza soka la kulipwa KCCA mwaka 2016, akizitumikia pia timu za taifa za vijana U20 na U23 za Uganda kabla ya kupanda timu ya wakubwa The Cranes mwaka 2019 na kudumu nayo hadi sasa.
Young Africans kwa misimu miwili mfululizo imekua na tatizo la beki wa kushoto tangu Gadiel Michael kuikacha timu hiyo na kutua Simba SC, jambo lililomfanya Kocha Nasreddin Nabi kumtumia beki wa kulia Shomari Kibwana au Winga Farid Mussa katika nafasi hiyo.
Sio kama Young Africans haina mabeki wa kushoto hadi kocha Nabi kuwatumia nyota hao, kwani kikosini mwake kuna David Bryson na Yassin Mustafa, ambao walikua wanasumbuliwa na majeraha ya muda mrefu, kiasi cha kushindwa kuwa Fit wakati wote.
Mbali na Mchakato huo wa usajili unaoendelea, pia Uongozi wa klabu hiyo upo kwenye mazungumzo na mastaa wake ambao mikataba yao inaelekea ukingoni, ili kuwaongezea mikataba mipya.
Mastaa hao wanaomaliza mikataba yao japo sio wote wanaoweza kusalia katika kikosi cha msimu ujao ni Nahodha Bakari Mwamnyeto, Shomari Kibwana, Saido Ntibazonkiza, Yacouba Sogne, Zawadi Mauya, Paul Godfrey ‘Boxer’ na Abdallah Shaib ‘Ninja’.