Kufuatia agizo lililotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kusaidiana na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), la kuzifungia baadhi ya nyimbo zilizokiuka maadili na kanuni za utangazaji na maudhui (2005), Roma Mkatoliki mkali wa wimbo wa Zimbabwe amefungiwa kwa muda wa miezi sita kutojihusisha na muziki baada ya kudharau wito wa Serikali.
Msanii huyo Ibrahim Mussa maarufu kama Roma Mkatoliki amekiuka maadili ya jamii ya kitanzania katika wimbo wake wa ”Kibamia”.
Kibamia ni wimbo ambao Roma Mkatoliki ameimba akiwa amemshirikisha Stamina na Maua Sama huku Dr.Shika akiwa kama ”video vixin” yaani mpendezesha video, maudhui ya wimbo huo hayaleti tafsiri nzuri kwa wasikilizaji hasa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambao bado hawajaanza kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, amesema kuwa Roma amedharau wito wa serikali ambapo leo aliitwa ili ahojiwe kutokana na wimbo wake huo ikiwa ni hatua ya pili mara baada ya Baraza la Sanaa Nchini Basata kumuita na kumtaka arekebishe baadhi ya sehemu katika wimbo huo.
“Tumempigia simu mara kadhaa hajapokea, tumemtumia meseji anasoma lakini hajibu chochote hivyo hiyo ni dharau na hatuendelei kudili na mtu mmoja wasanii ni wengi ambao wanahitaji msaada kutoka kwetu” amesema Shonza.
Mbali na kibamia jana TCRA, imetoa tangazo la kuzifungia nyimbo 15, zilizoimbwa na wasanii wa bongo fleva zikiwa na maudhui yaliyokiuka maadili ya Kitanzania hivyo, TCRA imevitaka vyombo vya habari nchini kutozirusha kupitia vyombo vyao vya habari.