Beki na Nahodha wa Kikosi cha Manchester United Harry Maguire ameonyesha kukasirishwa na kitendo cha kutolewa kwenye michuano ya Europa League, kwa kuchapwa na Sevilla CF mabao mawili kwa moja.
Man United walipata bao la kuongoza kupitia mkwaju wa penati uliopigwa na Bruno Fernandez dakika ya tisa, kabla ya Sevilla kusawazisha dakika ya 26 kupitia kwa Sergio Reguilon, huku Luuk de Jong akifunga bao la pili na la ushindi dakika ya 78.
Hata hivyo mlinda mlango wa Sevilla CF Bounou anapaswa kupewa sifa kubwa kwa kazi nzuri aliyoionyesha wakati wote wa mpambano huo, kwa kuzuia nafasi kadhaa za mabao na kuwatoa kabisa Man United.
Akizungumza na BT Sports baada ya mchezo huo, Maguire alisema “Kufungwa hakukubaliki. Kuishia hatua ya nusu fainali hakukubaliki. Kushinda mataji kunakaribia, tunahitaji kushinda mataji.”
“Timu bora imefungwa, wametuhukumu kwa nafasi tulizokosa. Tumefungwa kwa kona mbili kitu ambacho sio sahihi. Tulicheza vizuri na kustahili ushindi, tumeishia hatua ya nusu fainali kwa mara ya tatu msimu huu. Pengine ukosefu wetu wa uzoefu umetugharimu, tusingefungwa zile kona mbili.”
Naye Meneja wa Manchester United – Ole Gunnar Solskjaer alisema “Inahuzunisha, ni ngumu kukubali. Tumecheza vizuri na kutengeneza nafasi lakini hatukupata matokeo tuliyoyahitaji.”
“Tunahitaji kuboresha kikosi chetu, siwezi kusema lini au kama tutasajili lakini tunaliangalia hilo. Tunapaswa kuwa na uhakika wa 100% katika kutekeleza hilo.”
Kwa kupoteza nafasi ya kucheza Fainali ya Europa msimu huu. Sasa ni rasmi Manchester United wanamaliza msimu wakiwa wamecheza nusu fainali tatu bila ushindi. Katika Ligi Kuu Uingereza – EPL, Man United wamemaliza katika nafasi ya 3, alama 33 nyuma ya mabingwa Liverpool.