Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu ya Gwambina FC, imethibitisha kujiuzulu kwa mwenyekiti wa klabu hiyo Omary Mmasi, huku sababu za kujiuzulu kwa kiongozi huyo zikiendelea kuwa siri.
Mkuu wa idara hiyo Felician Mwenzi, amesema Uongozi umepokea barua ya kujiuzulu kwa Mmasi kwa masikitiko makubwa, na unaheshimu maamuzi yaliochukuliwa na kiongozi huyo mwandamizi.
“Ni kweli tumepata taarifa hizo lakini ni masikitiko kwani tupo katika mapambano makali kwa kipindi hiki kigumu tukisaka matokeo mazuri” amesema Mwenzi.
Mmasi amejiuzulu huku akiiacha Gwambina FC, ikiwa kwenye hali mbaya katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, licha ya kusaliwa na michezo kadhaa kabla ya kufikia ukingoni mwa msimu huu 2020/21.
Gwambina FC inashika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na alama 31.