Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Nzega vijijini, Hamisi Kigwangala amesema hakuwahi kuiba fedha za Serikali wala kujinufaisha binafsi kipindi alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter Kigwangala ameandika “Mimi sintosema chochote, nimemuachia Mungu apigane kwa niaba yangu. Nakubali ‘kuwajibika kisiasa’, siwezi kuwakana wasaidizi wangu, lakini sikuiba pesa wala kufaidika ‘binafsi’ kwa namna yoyote ile, lakini pia mimi sikuwa ‘afisa masuuli’ na hivyo sikuhusika na kuidhinisha pesa.”
Aprili 8, 2021 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere aliwasilisha ripoti ya mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo miongoni mwa Taasisi zilizofanya ubadhirifu wa fedha ni pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii wakati huo Waziri akiwa Hamisi Kigwangala.
Katika ripoti yake CAG alibainisha kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro zilifadhili Tamasha la Upandaji Mlima Kilimanjaro bila kuwepo kwenye bajeti.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa shindano la ‘Kigwangalla Kili Challenge’ la mwaka 2019 lilitumia Milioni 172 zilizotolewa na TANAPA na Ngorongoro.
Aidha, ripoti ya CAG ilieleza kuwa kituo cha televisheni cha Clouds kililipwa Sh629.7milioni na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kiasi cha Sh201.4 milioni kwa ajili ya kuonyesha matangazo ya tamasha la urithi lakini hakukuwa na risiti zozote za kielektroniki zilizotolewa kuthibitisha malipo hayo.