Umoja wa Mataifa UN, umetangaza kundi la viongozi vijana 17 kutoka pande mbali mbali duniani, ili kusongesha malengo ya maendeleo endelevu SDGs, hatua iliyofanyika wakati huu ambapo mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN, UNGA77 unaendelea.
Taarifa iliyotolewa jijini New York, Marekani na ofisi ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu vijana, imesema uteuzi huu hufanyika kila baada ya miaka miwili, kutambua vijana waleta mabadiliko ambao wanaongoza hatua za kukabili changamoto zinazokabili dunia na kuchagiza SDGs.
Kati ya vijana 5,400 waliochaguliwa ni 17 na uteuzi wa vijana hao yumo Mtanzania mjasiriamali wa tabia nchi, Gibson Kawago, aliyeshiriki shindano hilo kufuatia tangazo lililotolewa mapema mwaka huu la kusaka vijana hao ambapo majina 5,400 kutoka nchi 190 yaliwasilishwa.
Akizungumzia uteuzi huo, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa UN kwa vijana, Jayathma Wickramanayake amesema, “kundi hili la vijana viongozi wa SDGs kwa mwaka 2022 linajumuisha vijana ambao wanatekeleza hatua mbalimbali za uanaharakati wa vijana na uchechemuzi pindi linapokuja suala la kuhoji mamlaka na kujenga dunia bora kwa watu wote.”
Maeneo ambayo vijana hao wanahusika nayo ni maendeleo endelevu, haki za binadamu, amani na usalama na walio miongoni mwa waliochaguliwa wana umri wa kati ya miaka 17 hadi 29, wakiwemo wasanii, wanaharakati wa mazingira, wachechemuzi wa masuala ya jinsia, wabunifu na wengineo.