Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu, Zelote Stephen ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kumtafutia kiwanja cha nyumba, Bibi Georgina Kapilima ili waweze kujenga nyumba na kuishi bila ya bughudha.
Ushauri huo umetolewa baada ya bibi huyo kumuomba Mkuu wa Mkoa katika siku maalum ambayo Mkuu wa Mkoa aliiweka maalum kwaajili ya kusikiliza kero na maombi mbalimbali ya wananchi ambao walijitokeza kuzungumza moja kwa moja na Mkuu huyo.
Bibi huyo ambaye alianza kwa kuilaumu Halmashauri hiyo baada ya kufika katika ofisi hizo mara kadhaa akidai kutafutiwa kiwanja cha kununua baada ya kuona majumba yakiendelea kujengwa katika mji huo unaoendelea nae akiumia kwa kulipa kodi ya shilingi 45,000 kwa miezi mitatu, jambo ambalo linamuweka katika wakati mgumu kutafuta pesa ya kodi hiyo.
“Ombi la huyu bibi ni la msingi sana, maana kila kukicha anaona nyumba zinamea tu lakini yeye akihitaji kiwanja anaambiwa hakuna jambo ambalo halimuingii akilini, kwahiyo Mkurugenzi, na Katibu tawala fanyeni utaratibu huyu bibi apatiwe kiwanja aweze kujenga nyumba,” Zelote alieleza.
Awali alipokaribishwa kueleza shida yake mbele ya Mkuu wa Mkoa, Bibi Kapilima mwenye miaka 60 alisema kuwa kila akifika ofisi za halmashauri kuomba kiwanja anaambiwa hakuna huku akiona watumishi wa halmashauri hiyo wakiendelea kujenga majumba na kuongeza kuwa hataki kiwanja hicho bure na kuwa yupo tayari kukilipia ili nae awe na kwake.
Kwa kulipatia ufumbuzi jambo hilo katibu tawala wa Wilaya ya Nkasi, Festo Chonya alitoa ahadi ya kumpatia kikongwe huyo moja ya viwanja 35 vilivyopo karibu na Ikulu ndogo ya Wilaya ya Nkasi, Mjini Namanyere.
Mbali na kikongwe huyo Zelote alisikiliza kero za wananchi 14 kwa siku hiyo na kuweza kuzipatia ufumbuzi na wananchi hao kuondoka wakiwa wameridhika na maamuzi ya Mkuu wa Mkoa katika kutatua kero zao hizo.
Katika kusikiliza kero hizo Mkuu wa mkoa alikuwa na wakuu wa Idara za halmashauri hiyo, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa Wilay pamoja na baadhi wa wakuu wa idara kutoka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.