Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Huduma ya Afya kwa wote ni muhimu na Serikali itahakikisha kila Mwananchi anapata fursa ya huduma za afya ya msingi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya ufunguzi wa mkutano wa kumi wa Afya Tanzania na kuzindua Bodi ya wakurugenzi ya Tanzania Health Summit jijini Dar es Salaam.
Amesema, Serikali imeendelea kuwekeza katika Ujenzi wa Miundombinu ya Afya kwa kuongeza idadi ya vituo vya Afya na Hospitali, ambapo katika bajeti ya maendeleo ya Serikali mwaka wa fedha 2023/24 imetenga jumla ya shilingi bilioni 203.47.
“Fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali za Wilaya, vituo vya afya na zahanati pia shilingi bilioni 116.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya hospitali, vituo vya afya na zahanati pamoja kuongeza rasilimali watu,” amefafanua Rais Dkt. Mwinyi.