Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘TAIFA STARS’, Kim Poulsen amesema kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’, kimetokana na makosa yaliyofanyika kwenye safu yake ya ulinzi.
Taifa Stars ikiwa Uwanja wa Nyayo mjini Nairobi, katika mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki jana Jumatatu (Machi 15), ilipoteza kwa idadi hiyo ikiwa ni mchezo wa kwanza kwa kocha huyo kutoka nchini Denmark, tangu alipokabidhiwa mikoba ya Ndayiragije.
Paulsen amesema wachezaji wake waliofanya makosa mengi hasa kwenye safu ya ulinzi, hali ambayo iliwapa nafasi wapinzani wao kucheza kwa kujiamini na kupata bao katika vipindi viwili vya mchezo huo.
“Nimegundua kwamba tumepoteza kwa kuwa tumefanya makosa mengi upande wa ulinzi, hilo ni somo kwa ajili ya mechi zijazo ambapo tutafanyia kazi makosa hayo.”
“Pia wapo wachezaji ambao hawapo ndani ya kikosi watakapojiunga na timu itakuwa rahisi kwetu kuwa na upana wa kikosi zaidi hivyo safari bado inaendelea.” Amesema Kim Poulsen.
Taifa Stars itacheza mchezo mwingine wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Kenya keshokutwa Alhamis (Machi 18) mjini Nairobi. Kabla ya kuanza safari ya kuelekea mjini Malabo, Equatorial Guinea.
Michezo hiyo miwili ya kirafiki ni sehemu ya maandalizi kwa timu hizo za Afrika Mashariki, ambazo zinajiandaa na michezo ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2021).
Tanzania itacheza dhdi ya Equatorial Guinea (Machi 25) mjini Malabo, kisha itacheza dhidi ya Libya (Machi 30) jijini Dar es salaam, huku Kenya ikitarajiwa kucheza dhidi ya Misri (Machi 25) mjini Nairobi, na itamaliza dhidi ya Togo (Machi 30) mjini Lome.