Baada ya Kuambulia sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya DR Congo, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Kim Poulsen amesema mchezo huo wa kuwani kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022, ulikuwa mgumu lakini hana budi kuwapongeza wachezaji wake kwa kupambana.
Tanzania ilitanguliwa kufungwa bao katika mchezo huo uliounguruma mjini Lubumbashi, na baadae Mshambuliaji Simon Msuva aliisawazishia Taifa Stars na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kocha Poulsen amesema wachezaji wake walipambana wakati wote na walionesha kiwango kizuri, na matokeo yake wameondoka ugenini wakiwa na alama moja.
“Mchezo wetu ulikuwa mgumu hasa kutokana na wapinzani wetu ambao walikuwa bora na kuweza kumiliki mpira kwa muda kipindi cha kwanza na kupata bao ambalo tuliweza kusawazisha.”
“Kwa namna wachezaji walivyopambana wanastahili pongezi kwa kuwa wamefanya kazi kubwa dhidi ya mpinzani wetu ambaye alikuwa imara.
“Makosa yapo na tuliyafanyia kazi kipindi cha pili kuelekea katika mchezo wetu ujao dhidi ya Madagascar tutapambana kupata ushindi na tunaamini kwamba tutapata ushirikiano kutoka kwa mashabiki, ” amesema.
Tanzania (Taifa Stars) itaendelea na mchakato wa kusaka alama tatu muhimu za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia Septemba 7, Uwanja wa Mkapa, kwa kucheza dhidi ya Madagascar.