Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri usiozidi miaka 23, Kim Poulsen, ametaja kikosi cha wachezaji 20 kitakachoingia kambini kujiandaa na michuano ya ukanda wa Afrika mashariki na kati (CECAFA) inayotarajiwa kuanza mwezi huu.
Katika kikosi hicho kilichotajwa na Kim leo Julai 16, 2021 kwenye makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) idadi kubwa ya wachezaji ni wale wanaocheza kwenye timu zinazoshiriki Ligi Kuu msimu huu inayomalizika Jumapili.
Nyota hao ni makipa Metacha Mnata (Yanga), Daniel Mgore (Biashara Utd), na Wilbol Maseke (Azam Fc) huku mabeki ni Israel Mwenda, Lusajo Mwaikenda (KMC), Nickson Kibabage (Youssoufia fc), Paschal Msindo, Sospeter Israel (Azam) Abdulmajid Mangalo (Biashara Utd) Abdulrazack Hamza (Mbeya City) na Oscar Masai wa Ihefu.
Viungo ni Lucas Lucas Kikoti (Namungo), Joseph Mkele (Mtibwa Sugar),Rajabu Athuman, Meshack Abraham (Gwambina).
Wahambuliaji ni Erick Mwijage, Yusuph Mhilu (Kagera Sugar), Reliant Lusajo (Namungo), Andrew Semchimba (Ihefu) na Abdul Seleman ‘Sopu’ (Coastal Union).
Kim ameweka bayana kuwa hajawajumuisha wachezaji wanaocheza nje ya nchi kutokana na muda mchache wa maandalizi wakati Nickson Kibabage anayecheza Ligi Kuu ya Morocco amejumuishwa kutokana na kuwa yupo nchini Tanzania.
Reliant Lusajo, Mhilu na Sospeter (Bryson) ni wachezaji watatu waliozidi umri wa miaka 23 lakini wameitwa kwenye kikosi hicho kwa mujibu wa sheria inayoruhusu wachezaji watatu waliozidi umri kutumika kuongeza nguvu.
Timu hiyo itaingia kambini Jumatatu kujiandaa na michezo hiyo ambapo itacheza mechi mbili dhidi ya Congo DRC na Uganda kuanzia Julai 22, nchini Ethiopia.