Idara ya ujasusi ya Afghanistan imesema vikosi maalum vya Afghanistan vimemuua kiongozi muhimu wa kundi la Al-Qaeda, Abu Muhsin al-Masri ambaye pia alikuwa akitafutwa na Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya kitaifa ya usalama nchini Afghanistan, imeeleza kuwa Mmisri huyo aliyechukuliwa kama kiongozi namba mbili wa kundi la Al-Qaeda na mwenye ushawishi zaidi kwenye kundi hilo katika kanda hiyo ya India, aliuawa katika mkoa wa Ghazni katikati mwa Afghanistan.
Idara hiyo haikutoa maelezo zaidi juu ya operesheni hiyo iliyofanikisha kuuawa kwa kiongozi huyo wa Al-Qaeda ambaye jina lake liko kwenye orodha ya magaidi wanaotafutwa sana na shirika la upelelezi la FBI la Marekani.
Al-Masri alikuwa ameshitakiwa nchini Marekani kwa kutoa ufadhili wa bidhaa na rasilimali kwa shirika moja la kigeni linalohusika na ugaidi na pia, kwa njama ya kuwauwa raia wa Marekani.